OKama kuna mwezi ambao unaongoza kwa kulaumiwa na kulalamikiwa kwenye miezi 12 ya mwaka, basi ni mwezi Januari. Watu wengi huwa na malalamiko kuhusu mwezi huu, na hata wengine ambao hawana sababu zozote za kushindwa kufanya kitu, basi mwezi huu huwa sababu kwao.
Mwezi huu pia umekuwa unatumika kwa utani mwingi sana kuhusu mambo kuwa magumu na mwezi kuwa mrefu. Wapo wanaosema kwamba mwezi Januari una siku 40 badala ya siku 31. Wengine wanasema kwamba mwezi Januari ni mwezi ambao huwa unagoma kuisha. Ni utani lakini ndani yake unabeba kile ambacho watu wanapambana nacho.
Ni kweli kwamba mwezi Januari huwa ni mwezi mgumu kwa watu wengi, kutokana na mahitaji makubwa ya mwezi huo, lakini pia kutokana na mwezi unaokuwa umeutangulia mwezi Januari, yaani mwezi Disemba, ambapo watu wengi wanakuwa wamefanya matumizi makubwa sana kwenye sikukuu na mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Sina haja ya kurudia mahitaji haya ya mwezi Januari, wala ugumu wake, bali ninachotaka kukuambia leo ni kwamba, Januari imeisha. Japokuwa wengi wanaweza kushangilia kwamba Januari imeisha, lakini kuna Ujanuari ambao upo ndani ya wengi, na utaendelea kuwasumbua, na sasa watatumia jina na sababu nyingine badala ya kutumia Januari, kwa sababu imeshapita.
Leo ni siku ya mwisho kabisa ya mwezi Januari je unaamini kwamba kama Januari ilikuwa ngumu kwako basi leo ndiyo mwisho wa ugumu huo? Kwamba ukiamka kesho tarehe moja Februari basi kila kitu kitakuwa shwari? Kwamba kama ulikuwa huna fedha basi zitajaa kwenye mifuko yako?
Kama ndivyo unavyofikiria basi sina budi kukuambia kwamba unajidanganya. Na hilo siyo jipya, kwa sababu umekuwa na Januari nyingi kwenye maisha yako, na kinachofuata ni yale yale kwa jina tofauti.
Ninachokuambua rafiki yangu ni hichi, Januari imeisha lakini kuna ujanuari ambao upo ndani yako, na huu utaendelea kukusumbua kwa njia tofauti tofauti mpaka pale utakapokutana na Januari nyingine na uwe na sababu. Ninamaanisha kwamba, kama maisha yako yalikuwa magumu mwezi Januari yalikuwa hivyo siyo kwa sababu ya mwezi, bali kwa sababu yako wewe binafsi. Kwa kukosa mipango mizuri, au kwa kuwa na mipango ambayo siyo sahihi, umetengeneza matatizo kwenye maisha yako, ambayo umekuwa nayo kwa muda mrefu, na siyo tu mwezi januari. Hivyo basi, mwezi huu unaisha, lakini yale matatizo ambayo umekuwa unayatengeneza, utaendelea kuyatengeneza, kama hutachukua hatua kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Habari nyingine za kusikitisha kuhusu mwezi Januari ni hizi, unakumbuka ile tarehe 31 disemba na tarehe 1 januari ulikuwa unaimba nini? Unakumbuka ulivyokuwa unasema mwaka mpya mambo mapya? Unakumbuka ulivyojiambia makubwa kwa mwaka huu 2018? Hebu sasa niambie unaendeleaje na yale makubwa uliyokuwa umeyapanga. Je bado unayafanyia kazi? Hivi hata unayakumbuka? Maana tafiti zimekuwa zinaonesha kwamba, baada ya wiki tatu za mwanzo wa mwaka, asilimia 90 ya watu wanakuwa wameshasahau malengo waliyojiwekea kwenye mwaka mpya, wanakuwa wamesharudi kwenye maisha ya mazoea.
Hivyo kama na wewe rafiki yangu, ulipanga makubwa mwaka huu ulipoanza, lakini sasa hivi mwezi wa kwanza tu ndiyo unaisha na hukumbuki hata ulijiahidi utafanya nini, mambo yako yataendelea kuwa magumu.
Swali ni je, unawezaje kuhakikisha maisha yako yanakuwa bora wakati wote? Unawezaje kuishi yale maisha ya mabadiliko unayoyataka? Unawezaje kuepuka baadhi ya miezi kuwa migumu sana kwenye maisha yako?
Na maswali yote hayo yana majibu sahihi, na majibu hayo yanaanza na kitu kimoja, tengeneza mfumo wa maisha yako, ambao utauishi kila siku, ije mvua, lije jua, wewe utaishi mfumo huo.
Watu wengi wamekuwa wanashindwa kwa sababu wanategemea hamasa. Wanahamasika na kuchukua hatua fulani, lakini kwa sababu hamasa huwa haidumu, basi wanajikuta baada ya muda wanaacha kufanya na wanarudi kwenye mazoea. Lakini kama utatengeneza mfumo bora wa maisha yako, ukaufuata mfumo huo, basi maisha yako yatakuwa bora wakati wote. Hakutakuwa na tofauti kwenye maisha yako, iwe ni Januari au juni.
Unapotengeneza mfumo wa maisha, unaangalia yale maeneo muhimu sana kwenye maisha yako, ambayo unataka kupiga hatua. Yapo maeneo mengi, lakini mimi huwa napenda kuyagawa katika makundi matano muhimu. Makundi hayo ni maendeleo binafsi, kazi/biashara, fedha, afya na mahusiano.
Sasa huu ni mfano wa mfumo ambao unaweza kutengeneza na kuuishi kwenye maisha yako kila siku, na mfumo huu ukakuhakikishia unakuwa na maisha bora wakati wowote.
Maendeleo binafsi.
Kuwa na ndoto au maono makubwa ambayo unaishi kwa ajili ya kuyafikia. Kuwa na malengo na mipango ambayo unaifanyia kazi kila siku kwenye maisha yako. Halafu kila siku unapoamka, andika maono yako makubwa, pia andika malengo na mipango unayokwenda kufanyia kazi siku hiyo.
Andika vitu hivi kwenye kijitabu chako kila siku, na hii itaifanya akili yako kukuonesha fursa zinazoendana na kile unachotaka kufanya. Utaendelea kukumbuka maono yako makubwa, hata kama mambo yanaonekana kuwa magumu.
Kazi/ biashara.
Kama unafanya kazi, weka juhudi kubwa kwenye kazi hiyo, fanya kwa ubora wa hali ya juu sana, nenda hatua ya ziada kwa kufanya zaidi ya watu wanavyotegemea ufanye. Pia kazana kutoa thamani kubwa sana kwa chochote unachogusa.
Unahitaji kuwa na biashara, iwe una kazi au la, na kwenye biashara yako, kazana kutoa huduma bora kabia kwa wateja wako. Chagua tatizo ambalo linawasumbua watu, kisha weka juhudi kwenye kulitatua. Hakikisha maisha ya wengine yanakuwa bora wanapojihusisha na biashara yako.
Ishi kanuni hii muhimu sana ya kufikia uhuru wa kifedha kwenye maisha yako; mapato yawe makubwa kuliko matumizi, na kile kinachozidi, weka akiba na wekeza. Usikubali kabisa kutumia kila fedha unayoipata, utatengeneza matatizo. Hakikisha matumizi yako yanakuwa madogo kuliko kipato. Na hapa fanya vitu viwili, punguza matumizi na ongeza kipato.
Jilipe wewe mwenyewe kwanza, kwenye kila kipato unachoingiza, asilimia kumi usiitumie, hayo ni malipo yako, hupaswi kuyatumia kwa namna yoyote ile. Badala yake weka akiba na kisha wekeza ili izalishe zaidi.
Hakikisha unakuwa na mifereji mingi ya kipato, kipato chako kisitegemee eneo moja pekee. Kama umeajiriwa na unategemea ajira pekee kama njia ya kipato, umenasa kwenye mtego, kazana kujinasua kwa kuwa na mifereji mingine mingi ya kipato.
Mwisho kabisa kuhusu fedha, usikope kwa ajili ya kufanya sherehe, kula, kununua mavazi, kununua gari ya kutembelea, kujenga nyumba ya kuishi au kuanza biashara.
Afya ya mwili; kula vizuri, fanya mazoezi na pata muda wa kupumzika. Kila siku.
Afya ya akili; lisha akili yako chakula bora ambacho ni maarifa, soma vitabu, angalau kitabu kimoja kila mwezi, yaani kurasa 10 tu kila siku. Epuka habari hasi na za udaku, achana kabisa na habari zisizo na mchango wowote kwenye ukuaji na mafanikio yako.
Afya ya roho; Sali, tahajudi, kuwa mtu wa shukrani.
Kazana kuboresha mahusiano yako na wengine, hasa wale ambao ni wa muhimu sana kwako. Hapo unaanza na familia yako, unahitaji kutenga muda wa kuwa na familia yako, kusaidiana kwenye changamoto mbalimbali.
Pia boresha mahusiano yako na wengine wanaokuzunguka, kama wateja wako kwenye biashara, na hata jamii nzima unayoishi nayo.
Tengeneza mfumo wa kuishi kila siku kwenye maeneo hayo matano ya maisha yako, na hutakuwa na Januari ngumu kwenye maisha yako.
Rasilimali nilizokuandalia kuyafanya maisha yako kuwa bora mwezi Februari.
Karibuni Sana
By mr MIKAZI
0 Comments:
Post a Comment