KANUNI ZA FEDHA

KANUNI UNAZOTAKIWA KUZINGATIA KUHUSU FEDHA.
*KANUNI NO. 1*
Kamwe usikope fedha na hasa ya riba kwa ajili ya kuanzishia biashara (isipokuwa kwa mkopo ambao marejesho yake yanatokana na mshahara. Hii ni kwa sababu biashara huchukuwa muda mrefu kusimama yenyewe na kuanza kupata faida wakati marejesho ya mikopo mingi huanza mwezi baadaye ama hata kabla. Hivyo kamwe usikope mkopo ili
kuanzishia biashara ukitegemea hiyo hiyo biashara iweze kukulipia mkopo pamoja na riba yake.
*KANUNI NO 2*
Kamwe usitumie fedha ambayo bado  hujaipata / hujaimiliki. Wala usimuahidi mtu fedha kwa kutegemea fedha uliyoahidiwa na mtu mwingine. Usije ukamsikia mtu akikuambia "fulani njoo kesho ofisini kwangu saa 3 asubuhi uchukuwe shs. Milioni 2 halafu wewe akaenda dukani  kukopa vitu ukitegemea kulipa  utakapokuwa umechukua ile fedha uliyoahidiwa.
*KANUNI NO. 3*
Kama una nia ya kuweka akiba, kila upatapo fedha hakikisha huanzi kununua mahitaji yako kwanza kabla hujatenga fedha unayotaka kuweka akiba ukitegemea kwamba utaweka akiba kile kitakachobaki. Kwa kawaida huwa hakuna fedha inayobaki kwa sababu ilimradi fedha ya kutumia ipo, matumizi huwa hayakosekani na vitu ya kununua huwa vinaalikana lakini kama fedha ya kutumia haipo unaweza kutafuta njia nyingine ya kukabili changamoto zako. Ndiyo maana ni vema utaweka fedha ya akiba mbali kabisa na wewe na hiyo itakufanya ujione huna fedha kabisa.
*KANUNI NO 4*
Iwapo utapata fursa ya kukutana na watu mwenye mafanikio kiuchumi kamwe usiwaombe fedha. Waombe ushauri /waeleze  mawazo yako jinsi  unavyofikiri  namna utakavyofanya ili kupata fedha. Wanaweza wakaamua wao  mwenyewe hata kukupa fedha watakapoona kuwa mawazo yako ni mazuri na ya msingi. Lakini kamwe lengo lako lisiwe kupata fedha toka kwao.
*KANUNI NO 5*
Kamwe usitunze mbegu yako bila kuipanda. Watu wengi wanaishia kwenye kuweka akiba tu. Ni vigumu sana, kwa mfano kwa mfanyakazi, kuweka akiba tu na kupata mahitaji yote yatakayomfanya awe na kiwango kile kile cha maisha hasa hasa baada ya kustaafu. Unapoweka akiba hiyo ni mbegu; ipande. Unapoziweka tu mbegu nyingine huanza  kuoza (thamani yake huweza kupungua kwa sababu ya mfumuko wa bei na vitu kama hivyo.) Ndiyo maana ni vizuri kujifunza aina mbalimbali za uwekezaji unazoweza kutumia kukuza akiba yako. Hapa simaanishi kwamba lazima uwekeze kwenye biashara, kwa sababu unaweza kupoteza kirahisi fedha zako za akiba, hapa nazungumzia kuifanyia uwekezaji kama kununua hisa.
*KANUNI NO 6*
Kamwe usimkopee fedha mtu ambaye hutaki kumpoteza ama kukosana naye. Pale ambapo utamkopea hakikisha ndani ya moyo wako uwe umeamua kwamba ikitokea huyo mtu hajakulipa, hutakufa ukimnung'unikia huyo mtu. Wala hutampoteza huyo mtu kama rafiki. Kama utaona mtu utakaye mkopea anaweza akashindwa kurejesha mkopo na mkabaki marafiki basi mkopee. Lakini ukiona itakufanya hata  umchukie pamoja na hata ukoo wake tafadhali mshauri huyo rafiki aende  benki.
*KANUNI NO 7*
Kamwe usije akaweka sahihi yako kumdhamini mtu kwenye mambo ya fedha kama hutaki na hauko tayari kuja kumlipia huyo mtu hapo baadaye. Je unahitaji nieleze zaidi ya hapo kwa hili? Hapana, linajieleza lenyewe.
*KANUNI NO 8*
Epuka kuweka fedha ambayo hujapanga kuitumia  ndani ya kipindi kifupi sehemu ambayo inafikika kirahisi. Kwa mfano, usitembee na shs. Laki moja wakati ambapo ulichopanga kununua ama kufanya kinagharimu shs. Elfu ishirini tu. Utavikuta na kuvitamani  vitu ambavyo hukupanga kuvinunua ama kuvifanya.
* KANUNI NO 9*
Kamwe usitumie fedha kwa  kitu ambacho hakina ulazima kwako kwa wakati huo. Kabla hujatoa fedha yako kulipia kitu fulani hakikisha kwanza unajiuliza swali hili "kitatokea kitu gani kama sitanunua kitu  hiki?" Kama utaona unaweza kuishi vizuri na bila kuathirika na kukosekana  kwa kitu hicho tabasamu tu na ondoka zako,
* KANUNI NO 10*
Kamwe usifanye kitu ili kujionesha kuwa wewe ni tajiri. Kwa mfano kutumia shs elfu sabini kununua kitu kwa kuwa tu kinauzwa supermarket wakati kitu hicho hicho ungekipata Kariakoo kwa elfu thelathini. Kufanya hivyo ni kosa kubwa kikanuni isipokuwa kwa wale waliovuka kiwango cha hadhi ya kifedha kimaisha.
* KANUNI NO 11
Kamwe usiwe na tabia ya kutumia kipato chako chote ama zaidi ya kipato chako. Kufanya hivyo ni sawa na kuwa na tanki la maji lenye bomba dogo la kuingizia maji wakati hilo tanki lina  bomba kubwa la kutolea. Hata siku moja haliwezi kujaa. Na ikawa bomba la kuingizia maji litaendelea kupungua ukubwa wake ndivyo ambavyo tanki litaisha maji haraka. Lakini ukifanya kinyume chake yaani bomba kubwa liwe la kuingizia maji na lile dogo liwe la kutolea, hapo maji yatajaa na kufurika. Hivyo  hakikisha kila wakati na muda wote unaongeza ukubwa wa bomba linaloingiza na kupunguza bomba linalotoa.
*KANUNI NO 12*
Kamwe usiwe na mipango ya muda mfupi tu na kusahau kuwa na mipango ya muda mrefu pia na wala usikazanie kuwa mipango ya muda mrefu tu ukasahau kuwa pia na mipango ya muda mfupi. Dada mmoja aliambiwa ardhi ni mali. Basi akakusanya fedha kwa muda mrefu akanunua heka 30 za ardhi. Kwa sasa ana ardhi  lakini hana hela za matumizi wala za kuendeleza ardhi yake na haoni  hata jinsi ambavyo atatumia ardhi yake ili apate fedha hata kwa siku za usoni. Hebu jiulize; kuwa na heka 30 za ardhi huku huna fedha ya chakula kwa familia yako au ya kumpelekea mtoto wako hospitali huo ni utajiri au umaskini? Nadhani huyu dada alijali zaidi mipango ya muda mrefu akasahau mipango  ya muda mfupi. MUNGU TUBARIKI HAYA YAWE MEMA